Skip to main content

Mikopo inayotolewa na Halmashauri za Wilaya

CHINI YA SHERIA YA FEDHA YA SERIKALI ZA MITAA SURA. 290

UTANGULIZI

Mwongozo huu unaelezea kwa lugha nyepesi kanuni zilizowekwa chini ya sheria ya fedha ya serikali za mitaa chini ya kifungu cha 37 ambazo zinajulikana kama kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019 ambazo zinatumika katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa Tanzania Bara

UTOAJI NA UREJESHWAJI WA MIKOPO

Ni wajibu uliowekwa na sheria kwa Serikali za Mitaa kutenga asilimia kumi ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vyanzo vya ndani vya mapato kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vilivyosajiliwa vya;

 • wanawake,
 • vijana na
 • watu wenye ulemavu.

Katika kutenga fedha hizo mapato ya Mamlaka za Serikali za Mtaa yenye maelekezo maalum hayatahusika.

Katika kutekeleza wajibu wa serikali za mitaa kutenga asilimia kumi ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vyanzo vya ndani vya mapato Mkurugenzi atakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa:

 • Mamlaka ya Serikali za Mitaa inatenga asilimia kumi za mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo;
 • mikopo inatolewa kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa;
 • Vikundi vilivyokopeshwa vinarejesha mikopo kwa wakati

MGAO WA FEDHA ZA MKOPO

Mamlaka ya Serikali ya Mtaa zitatumia fedha zilizotengwa kwa mujibu wa Kanuni za kutoa mikopo kwa vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Mamlaka za Serikali za Mitaa zitatoa mikopo kwa kuzingatia mgawo ufuatao:

 • asilimia arobaini ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake;
 • asilimia arobaini ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya vijana; na
 • asilimia ishirini ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya watu wenye ulemavu.

MWONGOZO WA MIKOPO INAYOTOLEWA NA HALMASHAURI ZA WILAYA

CHINI YA SHERIA YA FEDHA YA SERIKALI ZA MITAA SURA. 290

Mikopo itakayotolewa chini ya kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu haitotozwa riba.

SIFA ZA KUPATA MIKOPO

 • Kikundi cha wanawake, vijana au watu wenye ulemavu kitakuwa na sifa ya kupata mkopo endapo:
 • kimesajiliwa kama kikundi cha wanawake, vijana au watu wenye ulemavu;
 • kinajishughulisha na ujasiriamali au kinakusudia kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati;
 • kwa kikundi cha wanawake au vijana kina idadi ya wanakikundi kuanzia kumi na kuendelea na kwa kikundi cha watu wenye ulemavu, kina idadi ya wanakikundi isiyopungua watano na isiyozidi kumi;
 • kina akaunti ya benki iliyofunguliwa kwa jina la kikundi kwa ajili ya matumizi ya kikundi; na
 • wanakikundi wake ni raia wa Tanzania wenye akili timamu na umri wa miaka kumi na nane na kuendelea; na
 • Kikundi hakitajumuisha wajumbe wenye ajira rasmi.
 • Kikundi kitahesabika kuwa kimepoteza sifa ya kupata mkopo endapo: –
 • kitapoteza moja wapo ya sifa zilizoainishwa hapo juu
 • hakijamaliza kurejesha mkopo uliotolewa na kimetoa taarifa za uongo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa lengo la kupata mkopo;
 • kimetumia fedha za mkopo kwa matumizi tofauti na yale yaliyoombewa mkopo bila ya idhini ya Mamlaka ya Serikali ya Mtaa; au
 • kimeshindwa kurejesha mkopo.

UTARATIBU WA UOMBAJI WA MKOPO

Mamlaka za Serikali za Mitaa zitawajibika kutoa tangazo kwa umma kwa madhumuni ya kuutarifu umma na vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuhusu kuwepo kwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi hivyo.

Kikundi kinachokusudia kuomba mkopo kitatakiwa kujaza fomu maalum itakayotolewa na Mamlaka ya Serikali ya Mtaa husika. Fomu ya maombi ya mkopo itaambatishwa na nakala za nyaraka zifuatazo:

 • katiba ya kikundi;
 • cheti cha usajili wa kikundi; na

MWONGOZO WA MIKOPO INAYOTOLEWA NA HALMASHAURI ZA WILAYA

CHINI YA SHERIA YA FEDHA YA SERIKALI ZA MITAA SURA. 290

 • kwa vikundi vinavyojishughulisha na biashara, leseni ya biashara; na nakala halisi za nyaraka zifuatazo:
 • taarifa ya akaunti kutoka katika benki ambayo kikundi kina akaunti;
 • barua ya utambulisho kutoka kwa Mtendaji wa Kijiji au Mtaa kwa kadri itakavyokuwa na Mtendaji wa Kata; na
 • wazo la biashara.

Baada ya kupokea maombi ya mkopo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitatakiwa kukiri kupokea maombi hayo ndani ya muda wa siku tatu tangu tarehe ya kupokelewa.

UTARATIBU WA UTOAJI WA MKOPO

Mamlaka za Serikali za Mitaa zitatakiwa kushughulikia maombi ya mikopo katika kipindi kisichozidi miezi mitatu tangu maombi hayo kupokelewa.

Endapo maombi ya mkopo yataridhiwa, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitatakiwa kuingiza kiasi cha mkopo kilichoridhiwa katika akaunti ya kikundi husika baada ya kusaini Mkataba na kikundi hicho.

Endapo maombi ya mkopo yatakataliwa, Mamlaka za Serikali ya Mitaa zitatakiwa kukitaarifu vikundi ambavyo maombi yake yamekataliwa kuhusu kukataliwa kwa maombi hayo pamoja na sababu za kukataliwa kwa maombi ndani ya muda wa siku saba tangu uamuzi wa kukataa maombi ulipofanyika.

MATUMIZI YA FEDHA ZA MKOPO

Fedha za mkopo zitakazotolewa chini ya kanui za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na zitatumika kwa miradi iliyoidhinishwa na Kamati ya Kudumu ya Fedha, Mipango na Uongozi kwa kuzingatia ushauri na mapendekezo ya Timu ya Menejimenti na Kamati ya Huduma za Mikopo.

Kikundi chochote kinaweza kubadilisha mradi baada ya kuomba na kupata idhini ya Kamati ya Kudumu ya Fedha, Mipango na Uongozi.

UREJESHAJI WA MIKOPO

Kila kikundi kilichopata mkopo kitatakiwa kurejesha mkopo baada ya miezi mitatu tangu siku ya kupata mkopo. Marejesho ya mkopo yatafanywa kila mwezi kwa kuzingatia viwango vilivyokubaliwa kati ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kikundi kilichopatiwa mkopo.

MWONGOZO WA MIKOPO INAYOTOLEWA NA HALMASHAURI ZA WILAYA

CHINI YA SHERIA YA FEDHA YA SERIKALI ZA MITAA SURA. 290

Mamlaka ya Serikali ya Mtaa inaweza kuingia makubaliano na kikundi kilichopatiwa mkopo kuhusu namna bora zaidi ya urejeshaji wa mkopo.

Mweka Hazina wa kikundi kilichopata mkopo atawajibika kuwasilisha marejesho ya mkopo kupitia akaunti maalum itakayoanzishwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kuwasilisha nakala ya hati ya benki kwa Afisa Maendeleo ya Jamii.

KUSHINDWA KUREJESHA MKOPO

Endapo kikundi kilichopata mkopo kitashindwa kurejesha mkopo katika muda uliopangwa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa itakipa kikundi hicho notisi ya siku thelathini ya kukitaka kikundi hicho kutoa sababu za kushindwa kurejesha mkopo kwa wakati.

Baada ya kumalizika kwa muda wa notisi iliyotolewa, Kamati ya Huduma za Mikopo itajadili kushindwa kwa kikundi kurejesha mkopo kwa wakati na kuishauri Timu ya Menejimenti hatua za kuchukua kwa mujibu wa Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Endapo tukio la kushindwa kurejesha mkopo kwa wakati limetokea kwa mara ya kwanza kwa kikundi, Timu ya Menejimenti inaweza kukiongezea kikundi hicho muda wa kurejesha mkopo husika.

Endapo kikundi kitashindwa kurejesha mkopo baada ya muda wa nyongeza, Mamlaka ya Serikali za Mitaa itatoa notisi kwa kikundi hicho kuhusu kusudio la kufungua shauri la madai dhidi ya wanakikundi.

NYONGEZA YA MUDA WA KUREJESHA MKOPO

Kikundi kilichopata mkopo kinaweza kuongezewa muda wa kurejesha mkopo huo kwa kuwasilisha maombi maalum kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa yakiainisha sababu za kushindwa kurejesha mkopo kwa wakati na mpango uliopo wa kurejesha mkopo katika muda wa nyongeza.

USIMAMIZI WA MIKOPO

Majukumu ya Afisa Maendeleo ya Jamii

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa atakuwa na majukumu yafuatayo:

 • kusajili vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu;
 • kuratibu mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye

MWONGOZO WA MIKOPO INAYOTOLEWA NA HALMASHAURI ZA WILAYA

CHINI YA SHERIA YA FEDHA YA SERIKALI ZA MITAA SURA. 290

 • ulemavu;
 • kupokea na kusajili maombi ya mikopo kutoka kwenye vikundi;
 • kusimamia uendeshaji na uhai wa vikundi pamoja na kufuatilia marejesho ya mikopo;
 • kuhakikisha mikopo inayotolewa inatumika kama ilivyokusudiwa;
 • kuratibu mafunzo ya vikundi;
 • kuandaa na kuwasilisha taarifa ya mikopo iliyotolewa kwa kamati ya Huduma za Mikopo;
 • kuandaa taarifa ya robo mwaka na kuiwasilisha kwenye vikao vya kisheria vya Mamlaka ya Serikali ya Mtaa; na
 • kuwa kiungo kati ya vikundi na Kamati ya Huduma za Mikopo; na atapokea na kusajili maombi ya mikopo kutoka kwa Afisa Vijana na Afisa Ustawi wa Jamii.

Katika kutekeleza majukumu yake Afisa Maendeleo ya Jamii atatakiwa kushirikiana na Maofisa wa Ustawi wa Jamii wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa

Kamati ya Huduma za Mikopo

Kamati ya Huduma za Mikopo katika kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa itakuwa na wajumbe wafuatao:

 • Mkurugenzi ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Kamati;
 • Mweka Hazina wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa;
 • Afisa Mipango wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa;
 • Afisa Ushirika wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa;
 • Afisa Ustawi wa Jamii wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa;
 • Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambaye atakuwa Mratibu na Katibu wa Kamati.

Kamati inaweza kumwalika mtaalamu yeyote kutoka ndani ya Mamlaka ya Serikali ya Mtaa ili aweze kuisaidia Kamati lakini mtaalam huyo hatakuwa na haki ya kupiga kura.

Majukumu ya Kamati ya Huduma za Mkopo

Kamati ya Huduma za Mkopo itakuwa na majukumu yafuatayo:

 • kuchambua na kujadili maombi ya mikopo yaliyopokelewa;
 • Kutoa ushauri na mapendekezo kwa Timu ya Menejimenti kuhusu vikundi vilivyokidhi vigezo vya kupata mkopo;
 • kutembelea na kukagua maendeleo ya vikundi vilivyopewa mikopo;
 • kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za vikundi vilivyopewa mkopo;
 • kusimamia na kufuatilia urejeshaji wa mikopo; na

MWONGOZO WA MIKOPO INAYOTOLEWA NA HALMASHAURI ZA WILAYA

CHINI YA SHERIA YA FEDHA YA SERIKALI ZA MITAA SURA. 290

 • kutekeleza suala lolote linalohusu utekelezaji wa Kanuni zilizowekwa kisheria kwa kadri itakavyoelekezwa na Timu ya Menejimenti.

Majukumu ya Timu ya Menejimenti

Katika kushughulikia maombi ya mikopo inayotolewa chini ya Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Timu ya Menejimenti itakuwa na majukumu yafuatayo:

 • kupokea na kujadili mapendekezo ya mikopo kutoka Kamati ya Huduma za Mikopo;
 • kutoa ushauri na mapendekezo kuhusu mapendekezo ya Kamati ya Huduma za Mikopo kwa Kamati ya Kudumu ya Fedha, Mipango na Uongozi; na
 • kuwasilisha taarifa ya robo mwaka ya utekelezaji wa Kanuni katika Sekretarieti ya Mkoa.
 • Majukumu ya Kamati ya Kudumu ya Fedha, Mipango na Uongozi

Katika kushughulikia maombi ya mikopo inayotolewa chini ya Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Kamati ya Kudumu ya Fedha, Mipango na Uongozi itakuwa na majukumu yafuatayo:

 • kupokea na kujadili taarifa ya mikopo kutoka Timu ya Menejimenti;
 • kuidhinisha mikopo kwa vikundi vilivyokidhi vigezo; na
 • kukagua miradi ya vikundi vilivyopata mikopo kwa kufuata utaratibu wa kawaida wa ukaguzi wa miradi ndani ya eneo la Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Majukumu ya Mkutano wa Halmashauri

Katika kushughulikia masuala ya mikopo, Mkutano wa Halmashauri utakuwa na wajibu wa kupokea, kujadili na kupitisha taarifa ya mikopo iliyoidhinishwa na Kamati ya Kudumu ya Fedha, Mipango na Uongozi.

Wajibu wa Mkaguzi wa Ndani

Mkaguzi wa Ndani wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa atakuwa na wajibu chini ya Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wa kukagua fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, urejeshaji na usimamizi wa mikopo hiyo.

Majukumu ya Sekretari eti ya Mkoa

Katika kusimamia masuala ya mikopo inayotolewa chini ya Kanuni za

MWONGOZO WA MIKOPO INAYOTOLEWA NA HALMASHAURI ZA WILAYA

CHINI YA SHERIA YA FEDHA YA SERIKALI ZA MITAA SURA. 290

utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Sekretarieti ya Mkoa itakuwa na majukumu yafuatayo:

kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatenga fedha kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 37A cha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa na Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa ajili ya kukopesha vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu;

 • kufuatilia na kutoa ushauri wa kitaalam kwa lengo la kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa huduma ya utoaji wa mikopo;
 • kuhakikisha fedha za mikopo zilizotengwa zinawafikia walengwa;
 • kutathmini utekelezaji wa mchakato mzima wa kutenga fedha za mikopo, utoaji na urejeshaji wa mikopo;
 • kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; na
 • kuwasilisha taarifa ya robo mwaka ya utekelezaji wa Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Majukumu ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Katika kusimamia utekelezaji wa Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa itakuwa na majukumu yafuatayo:

 • Kutoa tafsiri za sera na miongozo kuhusu usimamizi, utoaji na urejeshaji wa mikopo inayotolewa chini ya Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu;
 • kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ukusanyaji wa Mapato ya ndani kwa ufanisi;
 • kuhakikisha Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatenga fedha za mikopo kwa mujibu wa Sheria;
 • kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo zinawafikia walengwa;
 • kutathmini utekelezaji wa mchakato mzima wa kutenga fedha za mikopo, utoaji na na urejeshaji wa mikopo; na
 • kupokea taarifa ya robo mwaka ya utekelezaji wa Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka katika Sekretarieti za Mikoa.

MWONGOZO WA MIKOPO INAYOTOLEWA NA HALMASHAURI ZA WILAYA

CHINI YA SHERIA YA FEDHA YA SERIKALI ZA MITAA SURA. 290

Akaunti Maalum ya Mikopo

Kwa kuzingatia sheria na taratibu za usimamizi wa fedha za umma, kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa itatakiwa kufungua na kuendesha Akaunti Maalum ya Mikopo itakayofunguliwa katika mojawapo ya benki zinazotoa huduma katika eneo la Mamlaka ya Serikali ya Mitaa.

Mkurugenzi atakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya mikopo inayotolewa chini ya kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na fedha za marejesho ya mikopo hiyo zinahifadhiwa katika Akaunti Maalum ya Mikopo.

Mafunzo kwa vikundi

Mamlaka ya Serikali ya Mitaa itatoa mafunzo kwa vikundi vilivyokubaliwa kupata mkopo juu ya masuala ya uongozi, usimamizi wa fedha, uendeshaji wa miradi na utoaji wa taarifa hususani zinazohusu mkopo husika.

Makosa na adhabu

Mtu yeyote: –

 1. atakayetumia fedha za mkopo uliotolewa chini ya Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Kamati ya Kudumu ya Fedha, Mipango na Uongozi; au
 2. atakayetoa taarifa za uongo kwa lengo la kujipatia mkopo unaotolewa chini ya Kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,

Atakuwa ametenda kosa na endapo atatiwa hatiani atatozwa faini ya kiasi kisichopungua shilingi laki mbili na kisichozidi shilingi milioni moja au kutumikia kifungo kisichopungua miezi kumi na mbili na kisichozidi miezi ishirini na nne.

Mkurugenzi yeyote ambaye atashindwa kusimamia utekelezaji wa kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu atakuwa ametenda kosa la kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu inaweza, kwa kadri itakavyoona inafaa, kumchukulia hatua za kinidhamu.