Ijue Ardhi Kisheria
UTANGULIZI
Ndani ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania Ardhi ni eneo amabalo nimuhimu sana katika ukuzaji na uinuaji wa uchumi wa mwananchi mmommoja au vikundi.Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa eneo kubwa la nchi ya Tanzania halijatumika, hivyo basi kuna nafasi kubwa ya kila mwananchi kuweza kunufaika na hii Ardhi hasa kiuchumi. Sheria za Ardhi kwa Tanzania zimetawaliwa na sheria kuu mbili ambazo ni;
- Sheria ya Ardhi Sura 113 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002;
- Sheria ya Ardhi ya Vijiji Sura 114 ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Zipo sheria nyingine nyingi zinazohusu Ardhi ingawa tutajikita sana kuangalia sheria ya Ardhi Pamoja na marekebisho yake.
Umiliki wa Ardhi Tanzania
Ardhi yote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Ardhi ya Umma, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepewa dhamana ya kutunza na kumiliki Ardhi hiyo. Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha sheria ya Ardhi . Hivyo basi Ardhi yote ambayo iko ndani ya Mipaka ya Tanzania haimilikiwi na mtu awaye yeyote, japokuwa mtu anaweza kuwa na nia ya kumiliki Ardhi ambapo humilikishwa kwa muda wa kipindi cha miaka 33 au miaka 99 Hivyo basi Rais anaweza kunyang’anya Ardhi kutoka kwa mtu, shirika au kampuni yoyote, kwa ajili ya matumizi ya Umma.
Sheria ya ardhi imegawanya ardhi katika makundi makuu matatu,
- Ardhi ya jumla (General Land)
- Ardhi ya Kijiji (Village Land)
- Ardhi ya Akiba (Reserved Land)
Je, Raia asiye mtanzania anaweza kumiliki Ardhi?
Mtu anaweza kuwa na swali au dukuduku akilini mwake juu ya Mgeni ambaye siyo mtanzania kumiliki Ardhi ndani ya Tanzania. Sheria ya Ardhi iko vizuri kuwa mgeni ambaye sio mtanzania hawezi kumiliki Ardhi isipokuwa, pale ambapo atakuwa na mahitaji ya kuwekeza ndani ya nchi. Ambapo hawezi mtu huyu kujimilikisha Ardhi yeye mwenyewe kwa sababu tu anamahitaji ya kuwekeza La hasha! lazima apite kwenye Kituo Cha Uwekezaji Tanzania chini ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Act). Hili uhusisha pia makampuni ambayo yako Tanzania na kuendesha shughuli zake Tanzania lakini wanahisa sio raia wa Tanzania.
Njia za Kupata Ardhi Tanzania
- Kuna njia kadhaa zinazoonesha namna ya mtu anavyoweza kupata Ardhi ndani ya Tanzania ambazo ni;
- Kununua (Buying)
- Kurithi(Inheritence)
- Zawadi (Gift)
- Kusafisha ardhi (Cleaning a Virgin Land)
- Kutengewa (Allocation)
Kununua
Mtu yeyote anaweza kupata Ardhi ndani ya Tanzania kwa njia ya kununua Ardhi kutoka kwa mtu yeyote mwenye ardhi, kampuni au hata shirika lolote ndani ya Nchi. Ingawa manunuzi hayo ni kwamba yafanyike kisheria kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi. Kwa hiyo kila mtanzania anaweza kupata haki ya umiliki wa Ardhi kwa nia ya kununua kwenye sehemu yoyote ya Tanzania.
Kurithi
Namna nyingine ya kupata Ardhi ni kwa njia ya Urithi, pale ambapo mwenye ardhi amefariki na amemilikisha ardhi kwa wosia kwa kudhihirisha au kuweka wazi warithi ambao watarithi ardhi hiyo. Urithi unaanza kufanya kazi pale tu mwenye mali anapofariki.
Zawadi
Zawadi ni njia mojawapo ya mtu kuweza kumiliki Ardhi, hii hufanyika pale ambapo mtu mwenye Ardhi ameamua kutoa zawadi ya Ardhi kwa mtu mwingine, anaweza kuwa rafiki, au hata ndugu au wanaweza kupeana shirika na mtu, taasisi na taasisi.
Kusafisha Ardhi
Pia mtu anaweza kumiliki ardhi kwa njia ya kusafisha kichaka au msitu au Ardhi ndani ya Tanzania isiyokuwa na umiliki wowote, akafanya maendeleo ya moja kwa moja (permanent improvement) kwenye Ardhi hiyo. Maendeleo haya yanatakiwa kuwa kwa muda wa miaka kumi na mbili (12) mfulilizo bila kuhama au kuingiliwa na mtu mwingine na watu wengine wamefahamu mtu huyo kuishi hapo, hiyo Ardhi itakuwa ni ya kwake.
Kutengewa
Pia mtu anaweza kutengewa na kupewa Ardhi na mamlaka husika mfano mamlaka ya Kijiji, wajumbe wa sehemu husika kulingana na mamlaka ya eneo hilo. Lakini pia Rais wa Tanzania anaweza kutenga eneo na kumpa mtu au shririka mfano kuna uhitaji wa upanuzi wa Mbuga
Fulani ya wanyama, Rais anaweza kutenga eneo akawapa TANAPA au mamlaka yoyote inayohusika.
UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI
Taasisi zinazohusika katika utatuzi wa migogoro ya ardhi;
Kuna taasisi amabazo zipo kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya Ardhi ndani ya Tanzania Bara. Hivyo basi, taasisi hizo zimepangwa kwa utaratibu wa kisheria kulingana na mamlaka yake. Taasisi hizo zimeelezewa vizuri kwenye Sheria inayohusika na utatuzi wa Migogoro ya Arthi Sura na 216 ya mwaka 2002 (The Courts (Land Dispute Settlement) Act [ Cap 216 R.E 2002] ) na marekebisho yake .
- Halmashauri ya Ardhi ya kijiji (Village Council)
- Baraza la Kata (Ward Tribunal)
- Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya (The District Land and Housing Tribunal)
- Mahakama kuu kitengo cha Ardhi (The High Court Land Division)
- Mahakama ya Rufaa (The Court of Appeal)
Halmshauri ya Ardhi ya Kijiji
Kila kijiji ndani ya Tanzania kina Halmshauri inahohusika na utatuzi wa migogoro ya Ardhi. Ardhi ambayo inhusika na Halmshauri ni ile ambayo inatambulika kwenye Sheria ya Ardhi ya Kijiji. Ambapo Halmashauri ya kijiji ya Ardhi mjini haipo kabisa, kwasababu sheria za Ardhi zinazotumika kijijini na mjini ni tofauti. Halmshauri ya kijiji inaundwa na wajumbe saba, kati yao wajumbe watatu ni Wanawake na kila mjumbe anateuliwa na Halmashauri ya Kijiji na baadae kupitishwa na mkutano wa Kijiji.
- Kazi za Halmashauri ya Ardhi ya Kijiji ni kama zifuatazo;
- Kupokea malalamiko yanayohusu Ardhi
- Kufanya mikutano ya Usikilizaji wa migogoro hiyo
- Kufanya upatanishi juu ya watu wenye migogoro
Je, ni hatua gani yakufuata pale ambapo upande mwingine haujakubaliana na maamuzi? Katika mazingira haya upande ambao haujakuliana na maamuzi ya Halmashauri ya kijiji utapeleka rufaa kwenye Baraza la Kata, kwa ajili ya kutafuta suluhu zaidi.
Baraza la Kata
Baraza hili limeelezewa zaidi kwenye sheria ya mabaraza ya kata ya mwaka 1985 (The ward Tribunals Act, 1985). Tuangalie kwa ufupi juu ya Mabaraza haya ya kata. Mabaraza haya ya kata yana wajumbe wasiopungua wanne na wasiozidi nane. Ambapo watatu kati ya hao ni wanawake. Lengo kubwa au kazi kubwa ya mabaraza ya kata ni kuleta amani na utulivu katika eneo ambalo limeanzishwa kwa kutatua migogoro ya Ardhi iliyopo kwenye kata husika.
Katika kutatua migogoro Baraza la kata linaweza kuamua kuhairisha shauri husika kama njia ya kuelekea kutafuta upatanisho. Baraza la kata limepewa mamlaka kisheria kutatua migogoro ya Ardhi isiyozidi shilingi Milioni Hamsini za kitanzania, hii ni katika thamani. Katika uamuzi utakaofikiwa na Baraza la kata linaweza kuamua yafutayo;Kurejesha umiliki wa Ardhi
- Kutimiza jambo Fulani la kimkataba kufanyika
- Kuweka zuio la muda
- Kuamuru kutoa kiasi kilichodaiwa kwenye shauri
- Kuamuru malipo ya fidia kufanyika
- Kuamuru kulipwa kwa gharama zote zilizotumika katika kuendesha shauri kwa upande ulioshinda.
Pale ambapo Amri yoyote iliyotolewa katika Baraza la Kata itakapokuwa haijatekelezwa kwa upande unaotakiwa kutekeleza Amri hiyo, Baraza la Kata litapeleka shauri hilo kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ambayo Baraza hilo la Kata linapatikana.
Lakini pia upande ambao utakuwa haujaridhika na maamuzi yaliyotolewa na Baraza la Kata unaweza kuomba rufaa kwenda Baraza la Ardhi na Nyumba katika wilaya husika au eneo husika ndani ya siku Arobaini na tano kutoka siku ya hukumu ilipotolewa.
Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya
Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya linaongozwa na Mwenyekiti wa Baraza pamoja na washauri wasiopungua wawili (Assessors), hawa washauri kazi yao kubwa ni kutoa ushauri kwa mwenyeketi wa Baraza katika kufikia umauzi juu ya shauri husika. Ingawa katika ushauri wowote unaotolewa na washauri hawa, Mwenyekiti wa Baraza habanwi wala kufungwa na ushauri huo kwasababu kila uamuzi anaoutoa lazima aweke na sababu za kufikia uamuzi huo.
Katika hatua hii mlalamikaji au mlalamikiwa anaweza kuwepo mwenyewe mbele ya Baraza au kumtafuta wakili kwa ajili ya kumuwakilisha kwenye shauri la msingi. Ambapo lugha inayotumika katika Braza la wilaya ni Kiingereza au Kiswahili.
Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya linauwezo wa kupokea shauri lisilozidi Milioni mia tatu za fedha halali za kitanzania kwa mali isiyohamishika na Milioni Miambili Hamsini kwa fedha halali za kitanzania kwa mali ya inayohamishika.
Ni hatua gani ya kufuata ikiwa Baraza la Ardhi la Wilaya halijaanzishwa katika wilaya husika?
Katika mazingira haya sheria imeelekeza kwamba mlalamikaji anaweza kupeleka malalamiko yake kwenye Baraza ambalo liko karibu na wilaya hiyo mfano wilaya jirani au kama Baraza liko wilaya moja kwenye mkoa mzima, lazima kutumia Baraza hilohilo mpaka maelekezo yatakavyotoka vinginevyo.
Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya linapokea mashauri ya aina mbili kwanza kabisa ya rufaa kutoka kwenye Braza la Kata (Appeal from the ward Tribunal) au yanayokuja moja kwa moja kwenye Baraza hilo (Original Jurisdiction). Katika rufaa Baraza linaweza kufanya yafutayo
- Kukubaliana na hukumu ya Baraza la kata
- Kuamuru kurudiwa upya kwa shauri
- Kufuta shauri
katika hayo yote lazima sababu za msingi zitolewe kwa kina juu ya uamuzi huo
Mahakama Kuu Kitengo Cha Ardhi
Unaweza kushangaa kuwa Mahakama kuu kuwa na vitengo! ni kweli kabisa Mahakama hii ina vitengo mbali mbali kama vile;
- Kitengo cha Ardhi,
- Kitengo cha Kazi,
- Kitengo cha Biashara,
- Kitengo cha Kushughulikia wahujumu uchumi na Mafisadi; na
- Mahakama kuu yenyewe ambayo inaitwa kitaalam Masijala kuu (Main Registry).
Mahakama Kuu ya Ardhi inapokea kesi za rufaa kutoka Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya lakini yenyewe pia hupokea na kufanyia kazi malalamiko ambayo thamani yake isiyopungua Milioni mia tatu za fedha halali za kitanzania kwa mali zisizohamishika na Milioni miambili Hamsini kwa mali zinazohamishika.
Mahakama hii iko kikanda(zone) mfano kanda ya Pwani, kanda ya Tabora, lakini pia zingine zinakuwa zimewekwa mikoani kulingana na Muhimili wa mahakama ulivyoamua wenyewe katika uanzishwaji wa Mahakama kuu katika eneo Fulani la kimamlaka. Upande wowote katika shauri usiporidhika na maamuzi ya Mahakama Kuu unaweza kuomba kusudio la rufaa kwa ajili ya kupeleka shauri kwenye Mhakama ya Rufaa ya Tanzania.
Mahakama ya Rufaa
Hii ndio mahakama ya juu sana kwa Tanzania, yenyewe inapokea rufaa tu, haina mashuri ya awali isipokuwa inapokea mashauri ya rufani (Appellate cases) zinazotoka mahakama kuu.